Akizungumza katika kikao cha wazi cha bunge jijini Tehran siku ya Jumapili, Qalibaf alisema: “Tuhuma zinazotolewa kuhusu mivutano baina ya Marekani na utawala wa kibaguzi wa Kizayuni, pamoja na lugha ya dharau dhidi ya viongozi mashuhuri wa Iran, ni propaganda za kugeuza fikra za wananchi na kuathiri uwezo wa maamuzi wa taifa letu.”
Aliongeza kuwa: “Misimamo ya rais huyu mcheza kamari (Donald Trump) haina uzito wala uhalali wa kisiasa.”
Qalibaf alibainisha kuwa matamshi ya Trump ni sehemu ya mkakati wa vita vya kisaikolojia unaolenga kueneza hofu na kukata tamaa miongoni mwa wananchi wa Iran, pamoja na kudhoofisha umakini na busara ya viongozi wa taifa katika kufanya maamuzi ya kisiasa.
Spika huyo wa bunge pia alikemea taarifa zenye mkanganyiko na habari za uongo zinazotolewa na viongozi wa juu wa mataifa ya Magharibi, hasa kutoka kwa Rais wa Marekani ambaye alimtaja kuwa “kiongozi asiye na heshima wala hadhi.”
“Siku moja anatangaza kwamba amefuta vikwazo dhidi ya Iran katika ndoto zake bila hata kutoa tamko rasmi, na muda mfupi baadaye anatangaza kurejesha vikwazo hivyo kwa kisingizio cha msimamo wa viongozi wa Iran, kwa lengo la kuwafanya wananchi waamini kuwa viongozi wao ndio chanzo cha mateso.”
Qalibaf alihoji ni vipi Marekani ilianzisha vita vya uchokozi dhidi ya Iran huku ikiwa inaendeleza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Akasema: “Wairani hawataghairi kamwe katika kulinda ardhi na uhuru wao. Wasaliti na vibaraka wa maadui wataishia kwenye jalala la historia.”
Aliendelea kueleza kuwa: “Sasa ambapo vijana wa kizalendo wa Iran wamewavunja nguvu maadui, wapinzani wa maendeleo ya taifa letu wanatumia propaganda za kisaikolojia, jumbe za kupotosha, na matamshi yasiyo na maana kwa lengo la kuvuruga mshikamano wa kitaifa na kukamilisha ajenda yao ya zamani ya kutumbukiza Iran kwenye machafuko.”
Your Comment